Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kutoka Tehran, Ayatollah al-Udhma Makarem Shirazi, katika ujumbe aliouelekeza kwa wageni wa Mkutano wa Umoja wa Kiislamu, alisema: “Enyi wasomi, msitosheke kwa kuzungumzia umoja tu, bali leteni mbinu za kivitendo na za kudumu za kuutekeleza.”
Ujumbe wa Ayatollah al-Udhma Makarem Shirazi kwa Mkutano wa 39 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote, na rehma zimshukie Mtume Wake, rehema kwa viumbe vyote, Muhammad Mustafa (saw), na watu wa nyumbani kwake watoharifu pamoja na maswahaba wake wateule.
"Wale wanaomfuata Mtume, Nabii asiyejua kusoma wala kuandika, ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Torati na Injili; anawaamrisha mema na anawakataza maovu, anawahalalishia vitu vizuri na anawaharamishia vitu vibaya, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomuamini, wakamheshimu na kumsaidia, na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye – hao ndio wenye kufaulu."
(Surat Al-Araf: 157)
Mwanzoni mwa maneno yangu, napenda kutoa pongezi na salamu za heri kwa Waislamu wote, na hasa kwenu wageni wapendwa, kwa mnasaba wa kuzaliwa kwa rehema ya walimwengu, Muhammad Mustafa (saw). Vilevile, nawashukuru waandaaji na washiriki wote wa mkutano huu muhimu na mkubwa, na ninatarajia mkutano huu uwe hatua yenye athari katika kuleta mshikamano, ukaribu na umoja kwa Waislamu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya hii tukufu kwanza ameashiria majukumu makubwa ya Mtume, kisha akawataja wafuasi wake – wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakamsaidia, na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, ambao ndio wenye kufaulu.
Sifa hizo ndizo mambo ambayo umma wa Kiislamu unapaswa kuyafanya dira ya maisha yao. Ikiwa watajikusanya juu ya mhimili huu, na wakaimarisha imani zao, na kwa kila walichonacho wakamsaidia Mtume, na wakaifanya dini ya Kiislamu na Qur’an Tukufu kuwa kigezo cha maisha yao – nyoyo zao zitakaribiana.
Nyinyi nyote mnajua kwamba suluhisho la matatizo katika ulimwengu wa Kiislamu ni mshikamano juu ya mambo ya pamoja, japokuwa katika baadhi ya masuala miongoni mwa madhehebu ya Kiislamu kuna tofauti, lakini kusisitiza juu ya misingi na kushikamana na malengo ya pamoja ni ngome imara mbele ya njama za mafarakano, wanazuoni wa Kiislamu wanapaswa kwa umakini wasiruhusu tofauti na mgawanyiko baina ya Waislamu, leo hii, kuliko wakati mwingine wowote, umma wa Kiislamu unahitaji mno kurejea kwenye asili ya msingi na muhimu ya umoja, “Hakika huu ni umma wenu mmoja, na Mimi ni Mola wenu, basi niabuduni.”
Zaidi ya miaka miwili imepita tangu mashambulio dhidi ya moja ya mipaka muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu, yaani Beitul-Maqdis, na kumwagwa damu za kaka na dada zetu Waislamu huko Ghaza, na mtihani mgumu kwa ulimwengu wa Kiislamu, hususan wanazuoni wake, umejitokeza, njaa, kiu na mzingiro vimeenea kote katika eneo hilo, na kila siku mbele ya macho yetu – na hata macho ya ulimwengu mzima – watoto wanapoteza fahamu na akina mama wanadhoofika zaidi, huku ukatili na unyama wa utawala wa Kizayuni ukiendelea, hapa si suala tu la taifa moja lililodhulumiwa, bali ni kipimo cha dhamira ya ubinadamu.
Wajibu mkubwa wenu katika mkutano huu ni kwamba msitosheke kwa kuzungumzia tu umoja, bali toeni mbinu za kivitendo na za kudumu za kuutekeleza, miongoni mwa hayo ni: kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kitamaduni, kuunda jukwaa la pamoja la vyombo vya habari dhidi ya vita vya kisaikolojia vya adui, kuunga mkono kwa dhati taifa la Palestina, na kukabiliana na mipango ya kibeberu ya kuligawa umma.
Mimi ninatarajia kuwa mkutano huu utachukua hatua zenye manufaa katika kuleta mshikamano zaidi kati ya umma wa Kiislamu, na kwa ufupi, katika kuukuza na kuutukuza Uislamu na Waislamu, “Na Mwenyezi Mungu kwa yakini atamnusuru anayemnusuru Yeye, jakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda.”
Wassalaamu ‘Alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.
Qum Iran – Naser Makarem Shirazi
Maoni yako